Sherehe za kufungwa kwa Olimpiki Rio
Mashindano ya Olimpiki ya Rio yamemalizika rasmi, yakihitimisha siku 16 za matukio ya raha na karaha . Wakazi wa Rio walivumilia mvua na upepo mkali kushuhudia sherehe za mwisho za kufungwa kwa mashindano hayo.
Wakicheza densi aina ya Samba katika mitindo ya Ki-Brazil, wanamichezo mbali mbali pamoja na mashabiki waliaga mashindano hayo kwa mbwembwe za aina yake.
Wanariadha walimiminika katika uwanja huo wakipeperusha bendera za nchi zao katika msafara wa kuvutia huku wanariadha wa Brazil wakivalia viatu vilivyokuwa na nyayo zilizokuwa zikiwaka rangi tofauti kama vile nyekundu, nyeupe na samawati na mwanamiereka wa Tongan Pita Taufatofua akicheza jukwaani akiwa amevalia skati huku disco joka akicheza muziki na kuleta kumbukumbu ya wakati alipovutia umati mkubwa wakati alipopeperusha bendera ya nchi yake wakati wa sherehe za ufunguzi.
Kulingana na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Thomas Bach, mashindano hayo yalikuwa ya kuvutia katika mji wa kupendeza:
Kumbukumbu za michezo hiyo
Hata hivyo, michezo hiyo pia ilikuwa na kumbukumbu kwa wanariadha kutoka Brazil na wale wa nchi nyingine kote ulimwenguni. Timu ya kandanda ya Brazil iliicharagaza Ujerumani na kujishindia nishani ya dhahabu miaka miwili baada ya kushindwa kwa mabao 7-1 katika fainali ya kombe la dunia na kuwahuzunisha mashambiki wengi katika taifa hilo.
Mwanasakarasi wa Marekani, Simone Biles, alijishindia dhahabu 4, mwogeleaji Michael Phelps akaongeza nishani nyingine 5 na Usain Bolt akiwa ni mkimbiaji bora zaidi duniani akijishindia nishani 3 za dhahabu siku chache kabla ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa atakapohitimu miaka 30.
Baadhi ya changamoto
Lakini pia kulikuwa na matukio ambayo hayakuridhisha kama vile tukio la kutunga la mwogeleaji wa Marekani, Ryan Lochte, la kuvamiwa na maswala kama vile vidimbi vya maji katika mashindano hayo ya olimpiki kugeuka rangi kutoka samawati hadi kijani kibichi.
Sherehe hizo za kufunga mashindano hayo katika uwanja wa Maracana pia zilimaanisha kutimiza jukumu rasmi la kutia saini hatua ya kupokeza bendera kwa Japan itakayoandaa mashindano yajao ya Olimpiki katika majira ya kiangazi ya mwaka 2020.
Kuna matumaini kwamba mashindano ya Japan yatakuwa bora zaidi kuliko yalivyokuwa nchini Brazil lakini pia kuna wasiwasi kwenye nchini Japan iwapo mashindano hayo yatazidi kusambaratisha uchumi wa nchi hiyo ambao umekuwa ukijikokota kwa miaka mingi.
Gavana wa Japan alipokea bendera hiyo kutoka kwa Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Thomas Bach, na meya wa Rio Eduardo na kuashiria kukubalika Japan kuandaa mashindano hayo mwaka 2020.
No comments