Header Ads

Header ADS

LOWASSA AANDIKA WARAKA KUHUSU OPERESHENI UKUTA...AELEZA JINSI SERIKALI NA POLISI WALIVYOJIPANGA KUUBOMOA UKUTA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ameandika barua kuhusu operesheni ya chama chake iliyopewa jina la Ukuta na jinsi ambavyo jeshi la Polisi na Serikali lilivyopanga ‘kuubomoa’.

Katika waraka huo, Lowassa ameeleza kuwa ameamua kushika kalamu na kuandika masikitiko yake kuhusu hali ya amani nchini akidai Serikali imekata mkono wa amani.

Ameeleza kuwa Serikali imekandamiza upinzani na demokrasia na ndio chanzo cha wao kuanzisha UKUTA kupinga ukandamizaji huo.

“Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi watanzania walivyoipokea Operesheni hii, pamoja na vitisho vya dola,” ameandika. “Siku zote sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla ni wenye kulitakia amani na utulivu Taifa letu. Maandamano haya ya Septemba 1 ni ya amani, lakini vitendo vya jeshi la polisi vimewapa wasiwasi Watanzania,” Lowassa ameongeza.

Katika andiko hilo, Lowassa amedai kuwa amekuwa akipigiwa simu na viongozi wastaafu pamoja na watu mashuhuri wakimshauri kushawishi wakae na Serikali kuzungumza ili kuepusha taifa kujiingiza katika machafuko.
 
 Aliongeza kuwa kukutana na Rais John Magufuli katika Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa ni sehemu ya juhudi hizo.

“Nyote ni mashahidi wa tukio la kukutana na Rais Magufuli katika Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya mzee Mkapa. Ulikuwa ni mwanzo wa juhudi zetu za kuwanyooshea mkono wa amani. Lakini tunashangazwa wenzetu hawako tayari kuupokea mkono huo,” ameandika.

Aliongeza kuwa katika kikao cha juzi cha ndani cha chama hicho kilichofanyika katika Hotel ya Giraffe jijini Dar es Salaam walipanga kuzungumzia jinsi ya kuunyosha zaidi mkono wa amani lakini Jeshi la Polisi ‘liliukata’.

“Kitendo kile kwangu binafsi kimezidi kuniimarisha na kunipa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu katiba ambayo viongozi wetu waliapa kuifuata na kuitetea,” unasomeka waraka wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.

No comments

Powered by Blogger.