Header Ads

Header ADS

UNICEF: Njaa yatishia maisha ya watoto milioni 1.4

Nchini Yemen ambako kumekuwa na vita kwa takriban miaka miwili sasa, watoto 462,000 wanakabiliwa na mateso ya utapiamlo. Katika mashariki mwa nchi ya Nigeria, watoto 450,000 wamedhoofishwa na utapiamlo.
Takriban watoto milioni 1.4 kutoka Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen wanateseka kutokana na utapiamlo uliokithiri na wanaweza kufariki mwaka huu. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF. 

Katika taifa la Sudan Kusini, zaidi ya watoto 270,000 wanakumbwa na utapiamlo. Baa la njaa limeshatangazwa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo mfano eneo la kaskazini ambako wanaishi watoto 20,000. Idadi ya watu wasiokuwa na usalama wa chakula nchini humo inatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 5.5 ifikapo mwezi Julai endapo hakutachukuliwa hatua za kuzuia kuenea kwa ukosefu wa chakula na makali yake.
Mkurugenzi wa Shirika la Unicef Anthony Lake amehimiza juhudi za dharura zichukuliwe ili kunusuru maisha ya watoto walioko katika hatari. Mratibu katika shirika la hali ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa Eugene Owuso nchini Sudan Kusini anasema mambo mengi yamechangia kukithiri kwa njaa. "Mgogoro wa ukosefu wa chakula leo hii, umechangiwa pakubwa na mapigano, ukosefu wa usalama na watoaji misaada kukumbwa na changamoto ya kufikia maeneo yaliyoathiriwa. Pia huchangiwa pakubwa na mashambulio dhidi ya watoaji misaada mbali  na wizi wa misaada inayotolewa." 

No comments

Powered by Blogger.