KILICHOMPONZA KIGOGO WA TANESCO KUTUMBULIWA
HATUA ya Shirika la Umeme ya kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali, zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Felchesmi Mramba, ambaye jana amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye jana alisali mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma la mjini Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo ilisitishwa na Profesa Muhongo.
“Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi, hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya nishati hawakumuuliza hata Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,” alisema Rais.
Ateua bosi mpya
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa Mramba, amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akiwa kanisani, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Muhongo kwa hatua ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme.
“Namshukuru waziri wa nishati kwamba ameshatengua maamuzi hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda.” Rais Magufuli alisema haiwezekani watu mnapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati hii mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme hadi vijijini na umeme huo unaenda hadi kwa watu maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anakwenda kusimama kupandisha bei ya umeme.
Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya kupandishwa kwa bei ya umeme, Rais Magufuli alisema, “Na ndio maana baba askofu nalizungumza hili kwamba majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana naomba sana Watanzania muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni kwenda na wananchi wa kipato cha chini.”
Prof Muhongo alivyoikaanga Tanesco Juzi usiku
Profesa Muhongo alimwandikia barua Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi ya kumtaka kusitisha ongezeko la bei ya umeme iliyokuwa ianze kutumika jana. Profesa Muhongo alitoa uamuzi huo chini ya sheria ya umeme ya mwaka 2008 ambayo inampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya nishati.
“Leo Desemba 31, 3016 Ewura inaamuliwa kusitisha utekelezaji wa bei mpya za umeme uliyotangaza jana hadi hapo Serikali itakapopitia ripoti ya Ewura.”
Akizungumza na kituo kimoja cha radio jana, Profesa Muhongo alisema alisitisha uamuzi wa Ewura kwa sababu taratibu hazijafuatwa. Alisema pia Watanzania wote waliohojiwa walipinga ombi la Tanesco la kupandisha umeme.
“Ewura walitumia kigezo gani cha kuongeza bei, kama walitumia kigezo ambacho wengi hatukijui basi huo ni uamuzi wao wenyewe,” alisema.
Alisema taratibu zilizopo ni kwamba mara Tanesco wanapoomba kupandisha bei za umeme na Ewura ikishasikiliza maoni ya wadau, kabla ya kutangaza uamuzi ni lazima waziri mwenye dhamana na nishati ajulishwe kwanza.
“Lakini hivi ninavyozungumza na wewe hata mimi nilishtushwa jana naambiwa Ewura wametangaza, mimi nilikuwa sijapata chochote kutoka Ewura, mimi sijajadiliana na Ewura wala sijajadiliana na Tanesco kutokana na zoezi zima la kutaka kuongeza bei,” alisema.
Alisema waziri hashirikishwi ila anatakiwa kupokea taarifa ya mwisho, “hadi leo nimesikia tu, sijapokea hiyo taarifa, nenda kawaulize Ewura na Tanesco kama nina ripoti yao ya mwisho.
Alisema matatizo ya Tanesco hayatatuliwi kwa kuongeza bei, alisema matatizo ya shirika yanatokana na uongozi wa Tanesco na mambo mengine ambayo yanafahamika.
Alisema Ewura lazima ipeleke mapendekezo yake Wizara ya Nishati na Madini. Profesa Muhongo alisema hapo ndipo waziri atawaita Ewura na Tanesco kujadiliana na wakikubaliana hapo ndipo wataenda kutangaza hiyo bei.
Alisema haiwezekani Ewura ni chombo cha Serikali hivyo haiwezi kufanya bila waziri kufahamu.
Alisema tatizo la madeni ya Tanesco sio kuongeza bei ya umeme, alisema Serikali kwa sasa imefuta fedha za mikopo ya nje kwa ajili ya kulipa deni la Tanesco, hatuwezi kutafuta fedha za kulipa deni za kulipa madeni hayo kwa Watanzania halafu shukrani iwe ni kuongezewa bei ya umeme.”
Alisisitiza kuwa matumizi ya fedha ya Tanesco ni mabaya kwa sababu kila mwisho wa mwaka viongozi peke yake wanalipana bonus na akatoa mfano wa mwaka jana alifuta maamuzi hayo wakati tayari viongozi wameshapitisha uamuzi wa kulipana kati ya Sh milioni 60 na Sh milioni 40.
“Hivi kweli Tanesco wanafanya kazi nzuri, wanatuongezea bei ili walipane posho?” aliuliza.
Ahadi ya wizara kwa umma Waziri Muhongo akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2016/17 ya wizara hiyo bungeni mjini Dodoma mwaka jana kuhusu upatikanaji wa huduma ya umeme nchini, alisema kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme (access level), kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Watanzania waliofikiwa na huduma hiyo, ameongezeka kutoka asilimia 36 mwezi Machi 2015 hadi kufikia takriban asilimia 40 mwezi Aprili, 2016.
Alisema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali za kusambaza umeme nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kuhusu punguzo la viwango vya bei za umeme, Profesa Muhongo alisema Serikali imetekeleza ahadi yake ya kupunguza bei za umeme kuanzia Aprili Mosi mwaka 2016 kwa kati ya asilimia 1.5 na 2.4.
Alisema Serikali pia imeondoa tozo ya kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme (application fees) ya Sh 5,000 na tozo ya huduma ya mwezi (service charge) ya Sh 5,520 kwa Wateja wa Umeme kwa Daraja la T1 na D1, ambao wengi wao ni wa majumbani.
Hatua hii itawasaidia watumiaji wadogo wa umeme mijini na vijijini kumudu gharama hizo, hivyo kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi Ewura ilivyobariki ongezeko Juzi Ewura ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 badala ya asilimia 18.19 iliyokuwa imeombwa na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco).
Bei hizo mpya ilikuwa zianze kutumika jana Januari mosi, 2017. Akitangaza ongezeko hilo la bei, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura alisema, mamlaka yake imefikia uamuzi wa kuongeza asilimia 8.5 kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wake.
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linanunua umeme wa jumla kupeleka Zanzibar limeongezewa kwa asilimia 5.7 ya bei ya umeme.
Ongezeko hilo halikuwahusu wateja wa majumbani ambao matumizi yao hayazidi uniti 75 kwa mwezi ambao wengi ni wananchi wa vijijini ambao wanatumia umeme kwa kuwasha taa tu.
Sababu kupandisha umeme
Oktoba mwaka huu Tanesco iliomba kupandisha bei za umeme kwa maelezo kuwa gharama za uendeshaji katika uzalishaji na usafirishaji wa umeme zilikuwa juu hivyo kuna haja ya kupandisha bei za umeme.
Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni miezi saba tangu kutangazwa kwa bei mpya ya umeme iliyokuwa na punguzo la asilimia 1.5 hadi 2.4 sanjari na kuondoa tozo ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na gharama ya huduma kwa kila mwezi ambayo ilikuwa na Sh 5,520.
Wakati inaomba kupandisha bei aliyekuwa mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema ombi la mabadiliko ya bei za umeme ambalo waliliwasilisha Ewura Oktoba mwaka jana ni kutokana na agizo la kubadilisha bei za umeme la mwaka 2016 lililoanza kutumika Aprili 2016.
Alisema ifahamike kuwa bei za umeme zilitolewa zilitakiwa zitumike mpaka 31/12/2016, hivyo itakapofika Januari 2017 inatakiwa bei mpya za umeme kutolewa kwa mujibu wa sheria.
“Hivyo Taneso ilitakiwa kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme na kupeleka mapendekezo hayo kwenye Ewura ili kupitiwa na kufanyiwa taftishi, kupata maoni ya wadau ikiwa ni pamoja na baraza la ushauri la Serikali."
Hivyo basi ikiwa bei za umeme zitapanda au kutopanda, hiyo itategemea na mapitio ya tathmini ya gharama za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme tulizowasilisha Ewura.
Alisema Tanesco haiwezi kuamua yenyewe kupandisha au kutopandisha bei za umeme.
Aliongeza kuwa kupanda au kushuka kwa gharama za umeme ni suala la kisheria na ni jambo la kawaida kwani bei ya umeme imeshawahi kushuka katika vipindi tofauti.
Mramba alitoa mfano mwaka 2015 robo ya kwanza ya mwaka bei ilishuka kwa asilimia 2.5 na vivyo hivyo Aprili mwaka 2016 pia gharama za umeme zilishuka kwa asilimia 1.6.
Askofu Kilaini asifia Katika mahubiri yaliyoendeshwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, alipongeza jitihada za Rais Magufuli hasa kuhakikisha analeta usawa na uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali.
Askofu Kilaini alisema hali ya sasa kwa utendaji wa Serikali imebadilika kwani huko katika ofisi zaumma hakuna usumbufu wa kusubiria mtumishi, wala hakuna ile tabia ya kuombwa kitu kidogo “Ile kauli ya unatuachaje kama ilivyokuwa imezoeleka kwa baadhi ya watumishi katika sekta za umma sasa haipo tena.”
Kilaini aliwataka Watanzania kutumia sherehe za mwaka mpya 2017 kujitathmini na kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza hasa kwa mwaka uliomalizika 2016, hususani kama majanga ya tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka jana na kusababisha maafa makubwa mjini Bukoba.
“Tetemeko lililotokea Kagera sio nyundo ya kuwahimiza,bali ni kengele ya kutufanya tusonge mbele!hivyo,Watanzania tujielekeze kujituma kufanya kazi na asiyefanya kazi hana sababu ya kula,kama yalivyo maandishi ya kiroho,” alisema Askofu Kilaini.
Rais yuko mkoani Kagera kwa ziara yake ya siku mbili mkoani hapa pamoja na shughuli zingine atakagua miradi mipya inayojengwa na kuweka mawe ya msingi ambayo ni Shule ya sekondari ya Ihungo na zahanati ya Kabyaile ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi na kuzungumza na wananchi wa Kagera.
No comments