Header Ads

Header ADS

Taifa Stars yahitimisha mbio zake za kusaka nafasi ya kufuzu michuano ya AFCON


Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imehitimisha mbio zake za kusaka nafasi ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Super Eagles ya Nigeria.

Mchezo huo wa Kundi G ambao ulikuwa ni wa kukamilisha ratiba, umepigwa usiku wa leo nchini Nigeria na kushuhudia Taifa Stars ikipambana kutafuta heshima, licha ya matokeo ya mchezo huo kutomaanisha kitu chochote katika safari yake ya kufuzu Afcon

Kikosi cha Stars chini ya Kocha Boniface Mkwasa, na kuongozwa na nahodha Mbwana Samatta, kimeonesha ushindani kwa Nigeria na kulazimisha dakika 45 za kwanza kutoka nguvu sawa, licha ya mashambulizi makali kutoka kwa nyota wa Nigeria ambao wengi wao wanapiga soka la kulipwa barani Ulaya wakiongozwa na Ahmad Musa aliyesajiliwa hivi karibuni na klabu ya Leicester City ya England.

Kipindi cha pili hakikuwa na mabadiliko sana , lakini shukurani ziende kwa golikipa Aishi Manula ambaye amefanya kazi kubwa ya kupunguza idadi ya magoli kwa kuokoa michomo mingi hatari, ambayo huenda ingesebababisha hesabu kubadilika.

Licha ya uimara wa mlinda mlango wa Taifa Stars, kunako dakika ya 78 Kelechi Iheanacho alifanikiwa kutumbukiza mpira wavuni kwa shuti kali lililomzidi kimo Aishi Manula aliyekuwa ametoka kidogo nje ya msitari wa goli na kufanya ubao usomeke Nigeria 1-0 Tanzania.

Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta, alilazimika kutolewa nje baada ya kupata kashikashi zilizomsababishia maumivu dakika ya 85 wakati akigombea mpira wa kona, na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Ajibu.

Hadi dakika 90 zinamalizika, Taifa Stars ikiwa imepoteza mchezo kwa kupigwa bao 1-0 na kubaki na point yake 1, nyuma ya NIgeria yenye point 5 na Misri ambayo tayari imefuzu michuano hiyo ikiwa na point 10.

Kikosi cha Taifa Stars kilichoanza kilikuwa ni: Manula, Kapombe, Hussein, Andrew, Mwantika, Mao, Mkude, Kichuya, Msuva, Bocco, Samatta


No comments

Powered by Blogger.