Bastian Schweinsteiger atundika madaluga
Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Bastian Schweinsteiger aamua kutundika madaluga, kitisho cha kusambaa ugonjwa wa Zika katika michezo ya Olimpiki mjini Rio kiko chini,asema mkuu washirika la afya ulimwenguni WHO.
Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Bastian Schweinsteiger ameamua kuondoa mchango wake katika timu ya taifa. Mchezaji huyo wa kati mwenye umri wa miaka 31 anayesakata kandanda katika timu ya Manchester United ya England , ambaye alishiriki kwa mara yake ya 120 katika jezi ya Die Mannschaft katika mchezo wa nusu fainali wa Euro 2016 ambao Ujerumani ilishindwa kwa mabao 2-0 dhidi ya Ufaransa , amefichua taarifa hizo katika ukurasa wake wa Twitter jana Ijumaa. Schweinsteiger bado ana miaka miwili katika mkataba wake na United.

Maumivu ya goti aliyoyapata mwezi Januari mwaka huu yaliongezeka katika mwezi wa Machi , yakimzuwia kucheza katika klabu yake kwa ukamilifu na kufanikiwa kushiriki katika michezo michache tu kabla ya kucheza katika kinyang'anyiro hicho cha kombe la Ulaya , akifunga bao moja dhidi ya Ukraine katika mchezo wa kwanza wa Ujerumani katika kundi lake.
Mchezaji huyo kiungo mkabaji amesema sasa ni wakati muafaka wa kustaafu katika timu ya taifa kabla ya mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu kwa ajili ya michezo ya fainali za kombe la dunia mwaka 2018 dhidi ya Norway hapo Septemba 9, siku nne baada ya mchezo wa kirafiki nyumbani dhidi ya Finland.
"Nimemfahamisha kocha wa taifa Joachim Loew asinifikirie tena katika uteuzi wake wa timu ya taifa hapo baadaye kwa kuwa ningependa kuweka darini madaluga yangu nitumiayo kwa timu ya taifa" Schweinsteiger ameandika katika ukurasa wake wa Twitter. "Ningependa kuwashukuru mashabiki , timu, chama cha soka nchini Ujerumani na makocha.Katika mara 120 nilizoruhusiwa kucheza katika timu yangu ya taifa nilishuhudia nyakati ambazo haziwezi kuelezeka na za mafanikio makubwa," amesema Schweinsteiger.
Bastian Schweinsteiger ni mmoja kati ya wachezaji wanaoitwa wa kizazi cha dhahabu katika timu ya taifa ya Ujerumani , ambapo kimefanikiwa kuleta taji la kombe la dunia , mwaka 2014 kutoka Brazil. Ugonjwa wa Zika
Hatari ya ugonjwa wa virusi vya Zika katika michezo ya Olimpiki iko chini na inaweza kushughulikiwa bila matatizo , amesema mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, wiki moja kabla ya tukio hilo kuanza katika mji mkuu wa Brazil Rio de Janeiro.
No comments