Header Ads

Header ADS

Kapombe awa shukuru mashabiki, afunguka namna alivyoumia msimu uliopita

Baada ya kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa mashabiki msimu uliopita, beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amewashukuru mashabiki kwa kuonyesha imani naye na kumfanya awe mshindi wa tuzo hiyo.IMG_8070_0Nyota huyo ametwaa tuzo hiyo jana baada ya kujizolea jumla ya kura 203 kati ya zote 560 na kuwazidi wachezaji wenzake watano wa kikosi hicho, kipa Aishi aliyemuatia aliyepata kura 125, Farid Mussa (95), Ramadhan Singano (48), Himid Mao (45) na Pascal Wawa (44), kura 150 zilizofanya idadi ya kura zote kufikia 710 ziliharibika baada ya washiriki kukiuka vigezo na masharti.
Kapombe, 23, aliyecheza jumla ya dakika 3188 msimu uliopita katika mechi zote alizocheza Azam FC, hakufanikiwa kumaliza vema msimu baada ya miezi miwili iliyopita kuugua ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu) na kukosa sehemu yote iliyobakia ya msimu.
Pamoja na kuelezea furaha yake baada ya kutwaa tuzo hiyo wakati akifanya mahojiano maalumu na mtandao rasmi wa klabu yake ya .azamfc.co.tz.
Kapombe hakusita kuelezea namna alivyoumia msimu uliopita baada ya kuiona Azam FC ikishindwa kufikia malengo yake pamoja na yeye mwenyewe vivyo hivyo.
“Kwanza napenda kuwashukuru watu wote walionipigia kura na wale ambao hawakunipigia, vilevile napenda kuwashukuru wachezaji wenzangu ambao tumeweza kufanya kazi kwa pamoja mpaka ikaonekana kuwa mimi ndiye bora, ushirikiano ndio kilikuwa kitu kikubwa mpaka kikanipelekea mimi leo hii kuwa bora kama hivi, siwezi kuamini ubora wangu bila kuwepo wachezaji wenzangu.
“Pia napenda kushukuru sapoti ya mashabiki wote wa Azam FC waliyoitoa kwa timu na kwangu mimi, kwa namna moja ama nyingine imenipa mimi moyo na changamoto ya kufanya vizuri zaidi, nilipenda kufanya kizuri zaidi na zaidi kuliko hicho walichokiona kutoka kwangu, lakini napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kutoweza kumaliza msimu na yote hayo yaliyotokea ni moja ya sehemu ya maisha,” alisema.
Anazungumziaje kukosa sehemu muhimu ya msimu?
“Mimi nilijisikia vibaya kutokana na mimi kuwa mmojawapo wa wachezaji waliojiwekea malengo ya kuifikisha mbali Azam FC pale ilipotarajiwa na watu wengi, kama vile kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom, Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) na kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini ndoto zangu zote ziliweza kupotea.
“Lakini siwezi kulaumu sana kwa sababu ni kitu ambacho kilichotokea mbeleni, ila nimeumia zaidi kwa kuwa sikuweza kufikisha malengo ya msimu kwa namna tulivyojipangia,” alisema.
Aushukuru uongozi Azam FC
Kapombe pia alichukua fursa kuushukuru uongozi wote wa Azam FC kwa kumjali kwa kipindi chote alichokuwa akitoa mchango wake kwenye timu hiyo na hata alipopata matatizo na kudai kuwa amefarijika sana kwa hilo.
“Ninachowaahidi viongozi nna mashabiki nitaendelea kupigania timu kwa moyo mmoja na kuongeza juhudi zaidi ili kuweza kuifanya Azam FC ifike mbali zaidi,” alisema.
Amejipangaje kurejea tena dimbani?
Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, mwenye kasi ya kupanda mbele na kusaidia mashambulizi pamoja na kufunga, aliwaomba mashabiki, wachezaji wenzake pamoja na uongozi kwa ujumla uweze kumwombea kwa Mungu ili aweze kurejea tena dimbani msimu ujao.
“Kwa mashabiki, wachezaji wenzangu na viongozi nawaomba tu tuzidi kuombeana kheri, ili niweze kurudi vizuri na niweze kuimarika zaidi kiafya ili nifanikiwe kujiunga na wenzangu kwa maandalizi ya msimu ujao na kuifikisha timu katika malengo yale ambayo viongozi wamepanga,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Mashabiki wasiwe na wasiwasi hivi sasa naendelea vizuri baada ya kupat matibabu, na muda si mrefu natarajia kukutana na daktari wa timu kwa ajili ya kunipa maelekezo kuwa nini nifanye kwa sasa na kipi sitakiwi kufanya.”
Rekodi ya Kapombe 2015/16
Mbali na kukosa sehemu kubwa ya mechi za mwisho za msimu uliopita, Kapombe alifanikiwa kuwa beki pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom aliyeweza kufunga mabao mengi zaidi kwenye ligi akifunga nane na 12 katika mechi zote Azam FC ilizocheza hadi alipougua ghafla na kulazimika kukaa nje ya dimba kwa takribani miezi miwili hadi mitatu.
Pia ametoa pasi za mwisho saba na kuwa amekuwa ni mchezaji pekee wa Azam FC aliyepata Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi msimu uliopita, inayotolewa na mdhamini wa Ligi Kuu, Kampuni ya Vodacom, akitwaa ya mwezi Januari mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.